Amos 6

Ole Kwa Wanaoridhika


1 aOle wenu ninyi mnaostarehe na kuridhika katika Sayuni,
na ninyi mnaojisikia salama juu ya Mlima Samaria,
ninyi watu mashuhuri wa taifa lililoendelea kuliko mataifa mengine,
ambao watu wa Israeli wanawategemea!

2 bNendeni Kalne mkaone kutoka huko;
mwende hadi Hamathi iliyo kuu,
kisha mshuke hadi Gathi ya Wafilisti.
Je, wao ni bora kuliko falme zenu mbili?
Je, nchi yao ni kubwa kuliko yenu?

3 cMnaiweka mbali siku iliyo mbaya
na kuleta karibu utawala wa kuogofya.

4 dNinyi mnalala juu ya vitanda vilivyofunikwa kwa pembe za ndovu,
na kujinyoosha juu ya viti vya fahari.
Mnajilisha kwa wana-kondoo wazuri
na ndama walionenepeshwa.

5 eNinyi mnapiga vinubi kama Daudi,
huku mkitunga nyimbo za vinanda mbalimbali.

6 fMnakunywa mvinyo kwa bakuli zilizojazwa,
na mnajipaka mafuta mazuri,
lakini hamhuzuniki kwa maangamizi ya Yusufu.

7 Kwa hiyo mtakuwa miongoni mwa watu wa kwanza kwenda uhamishoni;
karamu zenu na kustarehe kutakoma.

Bwana Anachukia Kiburi Cha Israeli

8 g Bwana Mwenyezi ameapa kwa nafsi yake mwenyewe: Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote asema: “Nachukia kiburi cha Yakobo,
nachukia ngome zake;
nitautoa mji wao na kila kitu
kilichomo ndani mwake.”

9Kama watu kumi watabaki katika nyumba moja, wao pia watakufa. 10 hKama jamaa ambaye atachoma miili akija ili kuitoa nje ya nyumba, na kumuuliza yeyote ambaye bado anajificha humo, “Je, yuko mtu yeyote pamoja nawe?” Naye akisema, “Hapana,” ndipo atakaposema, “Nyamaza kimya! Haturuhusiwi kutaja jina la Bwana.”
11 iKwa kuwa Bwana ameamuru,
naye atabomoa jumba kubwa vipande vipande
na nyumba ndogo vipande vidogo vidogo.


12 jJe, farasi waweza kukimbia kwenye miamba mikali?
Je, aweza mtu kulima huko kwa maksai?
Lakini mmegeuza haki kuwa sumu
na matunda ya uadilifu kuwa uchungu:

13 kninyi mnaoshangilia kushindwa kwa Lo-Debari
na kusema, “Je, hatukuteka Karnaimu kwa nguvu zetu wenyewe?”


14 lMaana Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote asema,
“Nitainua taifa dhidi yenu, ee nyumba ya Israeli,
nalo litawatesa kuanzia Lebo-Hamathi
hadi Bonde la Araba.”
Copyright information for SwhKC